serikali ya wanafunzi Chuo kikuu cha Dar es salaam (DARUSO)

TAARIFA KWA UMMA
Serikali ya wanafunzi chuo kikuu cha Dar es salaam (DARUSO) imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kushambuliwa kwa risasi mbunge wa Singida Mashariki mhe.Tundu Antipas Lissu kwani kitendo hicho ni cha kikatili na kinyama kinyume na misingi ya umoja wa Taifa letu nje ya itikadi zetu ,dini zetu na tofauti zetu zingine huku tukitanguliza mbele maslahi ya taifa letu,utu,haki,heshima na usawa kwa watanzania wote. Kwani shabaha na madhumuni yetu watanzania ni kupigania maendeleo ya taifa letu na kujenga Tanzania yenye misingi ya haki,umoja ,upendo na mshikamano.
Rai yetu kwa Watanzania ni kuwa ni lazima tuweke pembeni maslahi ya itikadi za vyama vyetu,kuacha vijembe vyenye asili ya tofauti zetu za kiitikadi na tofauti zetu zingine na tulaani kitendo hiki kwa umoja wetu kama taifa.
Pia Tunaliomba jeshi la polisi kufanya kazi yake kwa weledi ili kubaini na kuhakikisha vitendo hivi vinakomeshwa mara moja na mwisho tunaungana na watanzania wote kumuombea mhe.Tundu Antipas Lissu kwa Mungu amponye na kuimarisha afya yake mapema iwezekanavyo.AMEN
Mungu ibariki Africa,Mungu ibariki Tanzania,Mungu ibariki Daruso
‘Whether right or left when it comes to the people’s lives we are one’
JILILI JOHN JEREMIAH
RAIS DARUSO
07/09/2017

DARUSO Yampongeza JPM kwa Kulinda Rasilimali za Nchi.

 

Rais wa Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO) akisisitiza jambo wakati wa mkutano na waandishi wa Habari uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam ukilenga kutoa tamko la DARUSO kuhusu kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali hasa matokeo ya Tume ya kuchunguza kiwango cha madini kwenye makontena 277.Kulia ni Waziri wa Ulinzi wa Serikali hiyo Bw. Richard Augustine na kushoto ni Waziri Mkuu wa Serikali hiyo Bw. Sintau Fredrick.
Na Frank Mvungi.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amepongezwa na Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (DARUSO) kwa kusimamia vyema rasilimali za Taifa ili ziweze kuwanufaisha watanzania wote.

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Rais wa (DARUSO) Bw.John Jilili wakati wa mkutano wao na vyombo vya habari uliolenga kutoa tamko la kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais kwa kuunda Tume iliyochunguza na kutoa matokeo kuhusu mchanga (makinikia) unaosafirishwa nje ya nchi.

“Kuanzia sasa uchakataji (processing) ufanyike hapa nchini na mikataba yote iwe na kipengele kinachoyalazimisha makampuni yanayopewa leseni ya kuchimba madini kuwa na mitambo ya kuchenjua makinikia ya madini yanayozalishwa na migodi hiyo.” alisema Jilili
Rais wa Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO) akitoa tamko lao mbele ya waandishi wa Habari kuhusu kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya Tano katika kuhakikisha kuwa watanzania wananufaika na rasilimali za madini.kushoto ni Waziri Mkuu wa Serikali hiyo Bw. Sintau Fredrick.
Akifafanua zaidi Jilili amesema kuwa mikataba yote ya Madini ni vyema ikatazamwa upya na kuzingatia maslahi mapana ya Taifa na si ya watu wachache, kwani kwa kufanya hivyo kuonyesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuleta mageuzi katika sekta ya madini nchini.

Katika mapendekezo yao DARUSO imebainisha kuwa Watanzania wangependa kuona Mikataba na Sheria zilizopo zinaruhusu ukaguzi wa mara kwa mara migodini ili Serikali ijiridhishe kuhusu kiwango cha madini kinachozalishwa katika migodi hiyo pamoja na Serikali kuwa na ubia wa asilimia 50 au 49 na wawekezaji katika sekta ya madini.

Aidha Jilili alisema vyema pia kwa vyema kwa Viongozi wote waliopewa dhamana ya kuwaletea wananchi maendeleo wakatekeleza wajibu huo kwa uzalendo na kuepuka kuingia mikataba inayowezesha kuiletea hasara Serikali.

“Tunapenda kuwaomba watanzania wote wasomi na wasio wasomi kumsaidia Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kufikia lengo lake la kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na hayo yanawezekana tu kwa kuweka uzalendo mbele na maslahi ya Taifa kwanza.” Alisisitiza Jilili

Aliongeza kuwa nidhamu na uwajibikaji katika sehemu za kazi ni jambo la muhimu kwa Watendaji waliokabidhiwa majukumu ya kusimamia sekta mbalimbali kwani kwa kufanya hivyo kutawezesha kuzaliwa kwa Tanzania mpya chini ya Uongozi wa Serikali ya awamu ya Tano.

“DARUSO inamthibitishia Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Watanzania wote kuwa iko sambamba nae katika harakati zake za kuikomboa nchi yetu katika Nyanja zote ikemo kiuchumi” Alisisitiza Jilili.

DARUSO haishangai juu ya matokeo ya tume iliyoundwa na Mhe. Rais Magufuli kwani inaamini kuwa kama utafiti haupo basi hakuna haki ya kuongea chochote.